17 Agosti 2020 - 09:38
Misri: Mazungumzo juu ya mzozo wa Bwawa la Renaissance kuanza tena kesho

Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Misri imetangaza kuwa mazungumzo juu ya mzozo wa ujenzi wa Bwawa la Renaissance juu ya maji ya Mto Nile yanatazamiwa kuanza tena kesho Jumanne tarehe 18 Agosti.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Misri imesema kuwa, kikao kilichofanyika jana cha mawaziri wa mambo ya nje na kilimo wa nchi tatu za Misri, Sudan na Ethiopia kimechukua uamuzi kwamba mazungumzo juu ya mzozo wa Bwawa la Renaissance yataanza tena kesho Jumanne kwa ajili ya kutafuta mwafaka wa kugawana maji ya Mto Nile na kuanza kazi bwawa hilo. 

Taarifa hiyo ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imesema kuwa, Cairo inasisitiza udharura wa kufanyika mazungumzo na kutiwa saini makubaliano baina ya nchi tatu za Misri, Ethiopia na Sudan kuhusu Bwawa la Renaissance kwa namna ambayo italinda haki za nchi zote tatu na kupunguza hasara zitakazosababishwa na ujenzi wa bwawa hilo kwa nchi mbili za Misri na Sudan. 

Misri na Sudan zinasema ujenzi wa bwawa hilo ambalo limegharimu karibu dola bilioni nne, utapunguza maji yanayofika katika nchi hizo na hivyo kuvuruga maisha ya mamilioni ya watu. Ethiopia nayo inasisitiza ujenzi wa bwawa hilo ni muhimu kwa ajili ya kueneza umeme katika nchi hiyo ili kuimarisha sekta ya viwanda na pia kuuza bidhaa hiyo katika nchi za nje.

Mazungumzo baina ya nchi hizo tatu yalikwama wiki iliyopita baada ya serikali ya Ethiopia kutaka mapatano ya kugawanya maji ya Mto Blue Nile yajadiliwe upya.

342/